User Rating: 0 / 5

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 

Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini wa TASAF katika Shehia ya Muyuni “B” Mkoa wa Kusini Unguja- Zanzibar wamepanda  Mbegu 15, 780 ya Mikoko ili kuhifadhi fukwe kama sehemu ya utekelezaji Miradi ya Kutoa Ajira za Muda.

Mtoa huduma za kitaaluma upandaji Mkoko katika shehia ya Muyuni B Bw. Suleiman Msabahah Othman ameeleza kuwa jamii katika shehia ya Muyuni B ilibuni na kuamua kutekeleza mradi huo kwa kuzingatia faida za mikoko katika fukwe za bahari akisema "Mikoko inazuia mmomonyoko wa kingo za fukwe wa bahari kwa kuzuia mawimbi, na upepo na pia mikoko inasaidia kuwapataia samaki maeneo ya mazalia na hivyo kuongezeka, pia mkoko hutoa tunda liitwalo Kaumwo linaloliwa na binadamu ambalo ni zuri kiafya kwani hutibu maradhi ya tumbo".

Mratibu Mkuu wa TASAF Zanzibar Bw. Ramadhan Madari alibainisha kuwa kuna zaidi ya aina 40 ya mikoko huku akizitaja aina chache zinazopatikana katika eneo la Muyuni kuwa ni Mkandaa (Ceriops tagal), Mui (Bruguiera gymnorriza), Magondi (Rhizophora mucronata), Mkomafi (Xylocarpus granatum), Mlilana (Soneratia alba) na Msikundazi (Heritiera litoralis).

Mratibu wa TASAF Unguja Fatma Mohamed Juma ameuelezea Mradi huo wenye walengwa 73 kuwa umetekelezwa katika kipindi cha kati ya mwezi Disemba 2014 na Januari 2015 na kugharimu kiasi cha shilingi 13,432,000.00.

Amefafanua matumizi kuwa Kati ya fedha hizo, jumla ya shilingi 10,074,000 zimelipwa kwa walengwa hao ikiwa ni ujira wao kwa kufanya kazi za mradi kwa kipindi cha mwezi wa 12, 2014 huku kiasi kingine cha shilingi 3,358,000 zikiwa ni gharama za vifaa kwa matumizi ya mradi huo kwa mwaka wa kwanza wa utekelezaji.

Akitoa taarifa ya utekelezaji katika uzinduzi wa Malipo ya Walengwa Kwa ajili ya Miradi ya Kutoa Ajira za Muda na kuwaongezea ujira walengwa wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Masikini katika Shehia ya Muyuni "B", Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Ladislaus Mwamanga amefafanua kuwa hadi sasa ni maeneo manane yakiwa ni halmashauri sita za Tanzania bara pamoja na Unguja na Pemba ndizo ambazo zimeanza kutekeleza miradi hiyo "kuna jumla ya miradi 544  inayotekelezwa katika maeneo manane ya utekelezaji kwa lengo la kuwapatia ujira walengwa wa mpango katika kipindi kigumu ili waweze kuvuka kipindi hicho wakipata mahitaji yao muhimu".

Kaimu Meneja Miradi ya Kutoa Ajira za Muda ambae pia ni mtaalamu wa mazingira wa TASAF Bw. Barnabas jachi ameainisha kuwa kiasi cha shilingi 12,036,753,844.82 zimetengwa na zitatumika ambapo katika fedha hizo kiasi cha shilingi 8,048,965,00.00 ni ujira kwa walengwa wapatao 58,965 katika vijiji 315 na shehia 40 watakaokuwa wakitekeleza miradi hiyo na zingine ni za uendeshaji, mafunzo na vifaa.

Akizindua Malipo ya Walengwa Kwa ajili Miradi ya Kutoa Ajira za Muda kwa Zanzibar ambayo ni ya kwanza kwa walengwa wa Shehia ya Muyuni "B", Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Dkt. Idriss Muslim Hija aliwahamasisha walengwa katika Shehia hiyo kuendelea kupanda na kutunza mikoko na akasema "wananchi na walengwa wa shehia ya Muyuni “B”, naamini kuwa Mradi huu wa Upandaji wa Mikoko Mtauthamini sana kwani utasaidia katika kutunza mazingira, hivyo natoa wito kuendelea kutunza mazingira ya bahari ili tuweze kunufaika na rasilimali hii sisi na vizazi vyetu vijavyo".

Pamoja na kutoa shukrani kwa mashirikiano ya karibu ya kisekta katika kuunga mkono juhudi za Serikali za Kupunguza Umasikini kwa wananchi wake Mkuu huyo wa Mkoa pia alitoa nasaha kwa walengwa akiwaambia "nawanasihi kutumia vizuri malipo ya ruzuku na hizi za Ujira wa kazi za Mradi mlizozifanya ili ziweze kuwafikisha katika malengo yaliyokusudiwa ya kuwatoa katika umasikini".

Dkt. Idriss alielezea Malengo mahsusi na ya msingi ya utekelezaji wa miradi ya Ajira za muda kwa walengwa kuwa ni kuwaongezea kipato ili kuziwezesha kaya husika kumudu makali ya maisha hasa katika kipindi kigumu cha kiangazi pia kuwawezesha washiriki kupata ujuzi katika stadi ambayo wanashiriki "tunatarajia, hapa Muyuni "B" baada ya utekelezaji wa mradi huu tutapata mafundi wa kutenda na hata kusimamia miradi ambayo inatekelezwa chini ya Mpango, aidha pia utekelezaji wa Miradi hii utaongeza rasilimali za Jamii na kuondoa kero kwa jamii ya kukosa huduma za kijamii katika maeneo yao" alibainisha Dkt. Idriss.

pic1Kaimu Meneja Miradi ya kutoa ajira ya mda mfupi wa TASAF Bw. Barnabas Jachi (wa kwanza kushoto) akitoa taarifa kwa Mkurugenzi wa Uratibu Ofisi ya Makamu wa pili wa Rais-OMPR Bw. Issa Ibrahim Mahmood (wa kwanza kulia) juu ya hali ya utekelezaji wa Miradi hiyo huko Zanzibar kabla ya kuhudhuria uzinduzu wa malipo ya Miradi ya Kutoa ajira ya Muda katika Shehia ya Muyuni "B", wa pili toka kulia ni  Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Ladislaus Mwamanga, Mkurugenzi wa Programu za kijamii wa TASAF Bw. Amadeus Kamagenge.

 pic2Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Ladislaus Mwamanga akitoa maelezo ya awali juu ya utekelezaji wa miradi ya kutoa ajira ya muda kabla ya uzinduzi rasmi wa malipo ya utekelezaji wa miradi hiyo uliofanyika katika shehia ya Muyuni "B" Mkoa wa Kusini Unguja

pic3

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Dkt. Idriss Muslim Hija akihutubia jamii katika Shehia ya Muyuni "B" wakati alipozindua malipo ya Miradi ya kutoa ajira ya muda Zanzibar.

pic4

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Dkt. Idriss Muslim Hija akimkabidhi mlengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini fedha za wakati alipozindua malipo ya walengwa kushiriki katika Miradi ya kutoa ajira ya muda katika Shehia ya Muyuni "B" Zanzibar

 pic5

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Dkt. Idriss Muslim Hija akiwa katika picha ya pamoja na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini na Uongozi wa TASAF Taifa kwenye Shehia ya Muyuni B wakati alipozindua na malipo ya Miradi ya kutoa ajira ya muda Zanzibar

pic6

Mtoa huduma za kitaaluma upandaji Mkoko katika shehia ya Muyuni "B" Bw. Suleiman Msabahah Othman (aliyeinama) akimuonesha Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Dkt. Idriss Muslim Hija (wa tatu kulia) namna mimea hiyo inavyopandwa wakati Mkuu huyo wa mkoa alipotembelea ufukwe wa Bahari katika shehia hiyo kujionea namna walengwa wa TASAF awamu ya tatu wanavyoshiriki katika miradi ya kutoa ajira ya mda mfupi kwa kuhifadhi mazingira na kupata ujira. Wengine wanaoshuhudia kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Ladislaus Mwamanga, Mkurugenzi wa Programu za kijamii wa TASAF Bw. Amadeus Kamagenge na Mkurugenzi wa Uratibu Ofisi ya Makamu wa pili wa Rais-OMPR Bw. Issa Ibrahim Mahmood.

Add comment


Security code
Refresh